![]() |
| Juma Luizio |
Na Arone Mpanduka
Mshambuliaji wa klabu ya Zesco United ya Zambia Juma Ndanda Luizio amesema anaamini Taifa Stars itaibuka na ushindi katika mchezo wa kesho dhidi ya Algeria.
Taifa Stars kesho itashuka dimbani kuikabili timu ya
taifa ya Algeria katika mchezo wa marudiano wa kuwania kupangwa kwenye makundi
ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za kombe la dunia za mwaka 2018.
“Cha msingi kocha Mkwasa apewe sapoti na Watanzania na siyo kummbeza kwa sababu ni Mtanzania mwenzetu.Tangu aichukue timu naona kuna utulivu wa hali ya juu uwanjani,”alisema.
Alisema anaiombea dua Taifa Stars na anaamini kesho itaibuka na ushindi huko Algeria.
Mshambuliaji huyo anasema majeruhi ya mara kwa mara yamemponza ndiyo maana kwa muda mrefu sasa amekuwa haitwi kwenye timu ya taifa.
Stars inayonolewa na kocha mzalendo, Charles Boniface Mkwasa iliwasili salama jana jioni katika mji wa Blida, uliopo takribani kilometa 75 kutoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Houari Boumediene jijini Algiers.
Taarifa kutoka huko zinasema wachezaji wote 21 wapo katika hali nzuri, hakuna mchezaj majeruhi hata mmoja, hivyo kocha Mkwasa ana wigo mpana wa kumtumia mchezaji yoyote anayemuhitaji kwa ajili ya mchezo huo wa kesho.
Mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018, utachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Mali na utaanza saa 1:15 usiku (Algeria) sawa na saa 3:15 usiku kwa saa nyumbani Tanzania na Afrika Mashariki.
Mchezo wa kwanza uliopigwa Jumamosi kwenye uwanja wa
Taifa jijini Dar es salaam, Stars ilibanwa mbavu kwa kutoka sare ya mabao 2-2,
matokeo ambayo yanaiweka Stars kwenye mazingira magumu ya kusonga mbele.
Katika mchezo huo wa kesho kama Stars inahitaji sare
inabidi ilazimishe sare ya mabao 3-3 ili iweze kusonga mbele na chini ya hapo
kama ikitoa sare ya mabao 2-2 itabidi timu zipigiane penati tano tano.
Ikiwa timu zitatoka sare bao 1-1 ama Stars ikashinda
ushindi njiti wa bao 1-0, Algeria itasonga mbele bila kikwazo kwasababu bado
watakuwa na faida ya mabao mawili ya ugenini.


0 comments:
Post a Comment