Kiungo Santi Cazorla wa klabu ya soka ya Arsenal na
timu ya taifa ya Hispania ameumia na sasa anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa
kipindi cha miezi minne kocha Arsene Wenger amethibitisha.
Wenger anasema Cazorla aliumia goti na kwamba
alifanyiwa scan Ijumaa hii na kugundulika atakua nje ya uwanja hadi mwezi machi
mwakani.
Santi Cazorla aliumia katika mechi ya sare dhidi ya
Norwich wiki iliyopita na kulazimika kucheza hivyo hivyo hadi mwisho wa mchezo
huku kocha Arsene Wenger akisema Cazorla alimaliza mchezo huo akiwa na mguu
mmoja.
Taarifa hizi ni mbaya na zinaumiza kwa mashabiki na
benchi la ufundi la Arsenal kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya majeruhi
ya wachezaji muhimu katika kikosi cha kwanza.
Mchezaji huyo anaungana na wengine kama Francis
Coquelin, Jack Wilshere, Theo Walcott ambao wote ni wa kikosi cha kwanza na
kumuacha Wenger akiwa na Mathew Flamini na Aaron Ramsey kuziba nafasi ya kiungo
baada ya nahodha Mikel Arteta pia kuwa majeruhi, sanjari na Alexis Sanchez huku
wakikabiliwa na mechi muhimu wanayohitaji ushindi ya klabu bingwa Ulaya dhidi
ya Olympiakos Pireus Jumanne hii.
Arsenal iko katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi
kuu nchini England nyuma ya vinara Leceister baada ya kuibuka na ushindi wa bao
3-1 dhidi ya Sunderland wikend hii lakini wanahitaji fomu kama hii Jumanne
katika usiku wa UEFA.

0 comments:
Post a Comment