Na Arone Mpanduka
Kufuatia kambi yake ya Ulaya kuota mbawa,bondia wa
ngumi za kulipwa nchini Francis Cheka amesema atafanya mazoezi yake hapa hapa
nchini ili kuhakikisha anamtwanga mpinzani wake Thomas Mashali siku ya Disemba
25 mwaka huu.
Cheka atavaana na Mashali katika pambano lisilo la
ubingwa litakalofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku lengo
likiwa ni kukata ngebe kwa pande zote mbili.
Akizungumza na mpanduka.blogspot.com kwa njia ya
simu kutoka Morogoro, Cheka alisema kuyeyuka kwa kambi ya Uingereza hakutoweza
kumfanya asijiandae dhidi ya pambano hilo.
“Nilipaswa kuwa Uingereza sasa hivi kujiandaa na
pambano dhidi ya Mashali lakini yote heri, nipo Morogoro na nitaendelea
kujiandaa nikiwa hapa na ninauhakika siku hiyo naua mtu,”alisema.
Alisema mipango ya safari yake ilikuwa inakwenda
vizuri lakini dakika za mwisho alishindwa kuelewa kilichotokea na kufanya
safari isiwepo tena.
Cheka alisema anashukuru kwamba kocha wake anampa
mazoezi ya kutosha na mbinu mbadala za kupata ushindi.

0 comments:
Post a Comment