Na Arone Mpanduka, Dar es salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua
kuingilia kati mgogoro wa kimaslahi unaoiandama klabu ya Stand United ya
Shinyanga na kutaka kamati iliyoundwa na mkuu wa mkoa wa Shinyanga kukaa
pembeni ili klabu hiyo isimamie yenyewe fedha za udhamini.
Mgogoro huo wa kimaslahi uliibuka baada ya kampuni
ya Acacia kujitokeza na kuidhamini timu hiyo na kisha mkuu wa mkoa wa Shinyanga
Ali Lufunga kuunda kamati maalum ya kusimamia fedha za udhamini kwa kuamini
kwamba zitatumika vizuri bila kuchakachuliwa.
Hata hivyo maamuzi hayo yaliibua mgogoro mkubwa
ambapo viongozi na wadau wa Stand walikuja juu na kushinikiza fedha hizo ziwe
zinapitia mikononi mwa klabu.
Akizungumza mapema leo hii Waziri wa Habari,
Utamaduni, Wasanii na Michezo Nape Nnauye alisema amezungumza na viongozi wa
klabu hiyo kuhusiana na sakata hilo na anaamini kwamba kukaa pembeni kwa kamati
hiyo kutaondoa mgogoro huo.
“Huenda Mkuu wa Mkoa alikuwa na nia njema lakini sasa
kwa hali jinsi ilivyo sasa inabidi yeye na Kamati yake wakae pembeni na suala
hili libaki mikononi mwa klabu,”alisema Nape.
"Ninadhani tatizo kubwa lilikuwa ni hilo, kwa hiyo tusubiri matokeo ya uamuzi huu na kisha tuone nini kitatokea"
Kwa upande wa uongozi wa Stand United umeelezea
kuridhishwa na uamuzi huo.
Mwenyekiti wa klabu hiyo Amani Vicent alisema kwa
hatua hiyo anaamini mgogoro uliopo utamalizika na timu itarejea katika kiwango
chake cha awali.
“Kuna wakati kiwango cha timu kilianza kushuka kwa
sababu ya hii migogoro lakini sasa naona itarejea kwenye uwezo wake wa awali,”alisema
Amani.

0 comments:
Post a Comment