Nahodha na mshambuliaji wa Manchester United Wayne
Rooney ameingia katika vitabu vya historia mara baada ya kuifungia timu yake
goli la ushindi dhidi ya mahasimu wao Liverpool katika mchezo wa ligi kuu
nchini England.
Goli hilo la Rooney lilikua ni la 176 kwake
akiifungia timu moja (Manchester United) na kumuacha mkongwe Thierry Henry
katika nafasi ya pili kwa magoli 175 yote aliyafunga akiwa Arsenal, huku kinara
wa mabao wa muda wote katika historia ya ligi kuu nchini England Alan Shearer
akibakia katika nafasi ya tatu na magoli 148 aliyoifungia Newcastle United
pekee.
Rooney ameendelea kujiweka katika wakati mzuri na
kulifanya jina lake lidumu katika vitabu hata atakapotundika daluga kutokana na
kuendelea kuvunja na kuandika rekodi zake mwenyewe, ambapo hadi sasa amekwisha
vunja rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa timu ya taifa ya England
huku pia akikaribia kuivunja rekodi inayoshikiliwa na Sir Bob Chalton ya
ufungaji bora wa klabu ya Manchester United.
Aidha katika mchezo wa jana dhidi ya Liverpool,
Wayne Rooney alifunga goli hilo la ushindi katika dakika ya 78 na kuwa ni goli
lake la ushindi kwa United dhidi ya Liverpool tangu alipofanya hivyo miaka 11
iliyopita mwaka 2005 katika uwanja wa Anfield.

0 comments:
Post a Comment