Na Arone Mpanduka
MTANDAO wa Wasanii Tanzania (SHIWATA) umeamua kumpa
uanachama wa heshima mchezaji bora wa Afrika, Mbwana Samatta pamoja na
kumzawadia ekari tano za ardhi katika kijiji cha Wasanii Mwanzega, Mkuranga kwa
ajili ya kuanzisha Chuo cha Mafunzo ya soka.
Mwenyekiti wa SHIWATA, Cassim Taalib alisema kuwa kikao
cha Kamati Utendaji ya Mtandao huo kilichoketi juzi kilifikia uamuzi huo baada
ya kufuatilia kwa karibu mafanikio ya Samatta akiwa na Timu ya Taifa ya
Tanzania 'Taifa Stars', TP Mazembe ya Jamhuri ya Kongo na kufanya vizuri katika
mashindano ya Afrika hadi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora Afrika.Alisema SHIWATA inatoa kiwanja hicho kama zawadi kwa mchezaji huyo kutokana na uwezo wake wa kulitangaza taifa katika medani ya kimataifa katika mchezo wa soka ambako wengine watafuata nyayo zake..
Taalib alisema taratibu za makabidhiano zinafanywa kwa
mawasiliano na baba yake mzazi, Ali Samatta na atakabidhiwa eneo hilo mara
baada ya kurudi kutoka Ubelgiji ambako anakwenda kusaini mkataba na timu ya KRC
Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji wa miaka minne.
SHIWATA yenye wanachama zaidi ya
8,000 inamiliki ekari 300 za kujenga makazi,kumbi za starehe, viwanja vya
michezo na nyumba za kuishi katika kijiji cha Mwanzega wilayani Mkuranga na
ekari 500 eneo la Ngarambe kwa ajili ya kilimo.

0 comments:
Post a Comment