Mshambuliaji wa timu ya soka ya Simba Hamis Kiiza
amezidi kuwa mtamu ndani ya kikosi hicho baada ya jioni ya leo kutupia mabao
mawili katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Burkinafaso ya Morogoro katika mchezo
wa Kombe la Shirikisho uliochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa timu hizo
kushambuliana kwa zamu lakini hakuna timu ambayo ilifanikiwa kupata bao hadi
dakika 45 za kwanza zinamalizika.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuliandama lango
na Burkina ambapo katika dakika ya 58 nusura Emery Nimuboma aipatie bao la
kuongoza baada ya mpira wake wa adhabu ndogo kugonga mwamba wa goli na kurudi
uwanjani.
Ikionekana kama vile mchezo huo ungeisha kwa sare ya
bila mabao, Hamis Kiiza 'Diego' aliwainua vitini mashabiki wa Simba baada ya
kuipatia timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi bao safi katika dakika ya 77 akimalizia
vema krosi ya Danny Lyanga.
Simba waliendelea kufanya mashambulizi kadhaa ambapo
dakika za nyongeza, Said Ndemla alifumua shuti kali nje ya eneo la 18 na
kufunga bao la pili. Dakika moja kabla mchezo haujamalizika Ndemla alifanyiwa
madhambi ndani ya eneo la hatari hivyo mwamuzi Andrew Shamba akaamuru ilipigwe
penati.
Kiiza alipiga penati hiyo na kuipatia Simba bao la
tatu.
Katika mchezo, wachezaji wa Burkina Hussein Shehe, Kessy Kessy, Jonathan Kishimba
na Ulimboka Mwakingwe walipewa kadi za njano huku kwa upande wa Simba ni Hija
Ugando na Hassan Kessy.
Simba iliwapumzisha Joseph Kimwaga, Mussa Mgosi na
Emery Nimuboma huku nafasi zao zikichukuliwa na Ugando na Lyanga na Mwinyi
Kazimoto. Burkina wao ilimpumzisha Kishimba na Hassan Mkota nafasi zao
zikichukuliwa na Jumanne Wida pamoja na Athuman Jumanne.
MECHI
ZINGINE ZA FA LEO(JUMAMOSI)
Pamba FC 1-4 Toto Africans- Uwanja wa CCM Kirumba,
Mwanza
Ndanda FC 5-0 Mshikamano FC- Uwanja wa Nangwanda
Sijaona, Mtwara.
MECHI
ZA FA KESHO(JUMAPILI)
Yanga vs Friends Rangers- Uwanja wa Taifa, Dar es salaam
Njombe Mji vs Tanzania Prisons- Uwanja wa Amani,
Njombe
Stand United vs Mwadui FC- Uwanja wa Kambarage,
Sinyanga

0 comments:
Post a Comment