Na Nicolaus Kilowoko
KATIKA hali ya kushangaza uongozi wa Klabu ya Stand
United ya Shinyanga umesema hauna taarifa yoyote juu ya kuondoka kwa wachezaji
wao Haruna Chanongo na Abuu Ubwa kwenda kufanya majaribio kwenye timu ya TP
Mazembe ya Congo DR.
Hivi karibuni wachezaji hao walitimkia katika klabu
hiyo ya Congo DR kwa ajili ya kufanya majaribio ya siku 10, zoezi ambalo
walilifanya na hatimaye kufanikiwa kufuzu huku hivi sasa wakiwa wanasubiri kauli
ya mwisho kutoka kwa mmiliki Moise Katumbi.
Lakini leo hii klabu ya Stand United imesema imekuwa
ikisikia tu kwenye vyombo vya habari juu ya wachezaji hao lakini haina taarifa
yoyote rasmi kuhusiana na kuondoka kwao.
Akizungumza na MPANDUKA BLOG, msemaji wa Stand
United, Deo Kaji Makomba amesema kocha mkuu wa timu hiyo Patrick Liewig
amemwambia kwamba katika meza yake hakuna taarifa yoyote juu ya kutokuwepo kwa
wanandinga hao.
“Kocha Liewig amenidokeza kwamba anashangazwa na
kitendo cha wachezaji hao(Chanongo na Ubwa) kutojitokeza mazoezini kwa kipindi
kirefu, tena bila taarifa yoyote,”alisema Makomba.
Uongozi wa Stand unaonekana kuleta sintofahamu kwa sababu
hivi karibuni wakala wa wachezaji hao alizungumza na vyombo vya habari na
kukiri kwamba kila kitu kilikwenda sawa na kwamba waliwasiliana na uongozi wa
Stand juu ya safari ya wachezaji hao.

0 comments:
Post a Comment