Yanga leo imeisambaratisha bila huruma Majimaji ya
Songea kwa kuichapa mabao 5-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom uliochezwa
katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
Thaban Kamusoko aliwashtua Majimaji kwa bao la mapema
la dakika ya nne akitumia pasi nzuri ya Deus Kaseke.
Baada ya bao hilo Majimaji inayonolewa na Kalimangonga
Ongala ilionyesha utulivu hasa kwenye eneo la kiungo hali iliyopelekea timu
hizo kwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao hilo moja pekee.
Kipindi cha pili Yanga iliingia kwa nguvu mpya na
katika dakika ya 47 tu Kamusoko alimtengenezea bao safi Donald Ngoma
aliyeiandikia Yanga bao la pili.
Baada ya bao la pili Majimaji walianza kupoteana ndipo
mshambuliaji hatari Amissi Tambwe alipoanza kutoa adhabu kali kwa Majimaji
akifunga bao la tatu katika dakika ya 57 kwa pasi ya Ngoma kabla Kaseke
hamjamtengenezea bao jingine kwenye dakika 72.
Ikionekana kama vile pambano hilo lingeisha kwa Yanga
kuibuka na ushindi wa mabao 4-0, beki wa Majimaji Sadick Gazza alimzawadia
Tambwe bao la tatu kwake na la tano kwa Yanga katika dakika ya 84 baada kufanya
uzembe wa kujiangusha na Tambwe akaunasa mpira huo na kumchambua kipa David
Burhan.
Kwa ushindi huo Yanga imerudi tena kileleni kwa
kufikisha pointi 39 sawa na Azam lakini ikiizidi kwa tofauti ya mabao ya
kufunga na kufungwa.
Katika michezo mingine ya ligi kuu leo, Mwadui FC
iliyokuwa nyumbani imeifunga Kagera Sugar mabao 2-1 wakati huko Tanga African
Sports imetoka sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar.

0 comments:
Post a Comment