Na Arone Mpanduka
Siku moja baada ya Mbwana Samatta kurejea katika klabu
ya TP Mazembe badala ya kwenda Ulaya kujiunga na Genk ya Ubelgiji, meneja wa
mchezaji huyo Jamal Kisongo ametoa sababu tatu za maamuzi hayo.
Baada ya kushinda tuzo yake ya mwanasoka bora kwa
wachezaji wanaocheza ndani ya Bara hilo, Samatta ambaye ni mshambuliaji wa TP
Mazembe ya Congo DR na timu ya taifa, Taifa Stars alitarajiwa kusafiri kwenda
Ulaya lakini safari yake ilikwama kufuatia klabu hiyo ya Ubelgiji kushindwa
kuafikiana dau na mmiliki Moise Katumbi.
Genk walikuwa wanataka kumsajili Samatta kwa dau
ambalo mmiliki huyo wa TP Mazembe hakuridhika nalo kwa madai kwamba bei hiyo
hailipi.
Akizungumza na MPANDUKA BLOG, Kisongo alisema baada ya
Katumbi kuonekana kushikilia msimamo wake wa kutomruhusu Samatta kwenda Genk,
ndipo akaamua kumshinikiza nyota huyo arudi kwenye klabu yake ili amalizie
mkataba wake na baada ya hapo aondoke akiwa kama mchezaji huru.
“Hiyo ni sababu ya kwanza ambayo tunaona kwa kufanya
hivyo Katumbi lazima atakataa kuona Samatta anaondoka klabuni hapo akiwa kama
mchezaji huru, jambo ambalo halitompa faida mmiliki huyo,”alisema Kisongo.
Alisema sababu ya pili ni kitendo cha udhalilishaji
kilichotokea hivi karibuni cha gazeti moja la udaku kuandika kwamba Samatta
alifumwa hotelini akiwa na mwanamke, hivyo wameona ni vema kumpeleka Congo ili
kuepusha madhara yatakayotokana na kuharibiwa kwa saikolojia yake kufuatia
habari hizo za uzushi.
Alisema kitendo cha Samatta kuendelea kukaa nchini
kingezidi kutoa mwanya kwa magazeti ya udaku kumchafua na hivyo kuzima kabisa
ndoto zake za kusonga mbele.
Kisongo alisema sababu ya tatu ni kumfanya nyota huyo
asikae bila ya kuwa na mazoezi, hivyo ni bora aende Congo kufanya mazoezi na
wenzake huku Katumbi akiwa anatafakari nini cha kufanya juu yake.

0 comments:
Post a Comment