Timu ya taifa ya Tanzania Bara Kilimanjaro Stars leo
imeshindwa kusonga mbele katika michuano ya Chalenji baada ya kutolewa nishai
na timu ya Ethiopia kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-3 katika mchezo wa
robo fainali uliopigwa mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.
Katika mchezo huo Kili Stars ilikuwa ya kwanza
kupata bao lililofungwa na John Bocco katika dakika ya 24 ya mchezo.
Bao hilo lilipeta hadi dakika ya 57 ambapo Ethiopia
walisawazisha kwa mkwaju penati uliofungwa na Panom na kufanya sare ya bao 1-1.
Sare hiyo ilidumu hadi dakika ya 90 zinamalizika na
kwamujibu wa kanuni za mashindano hayo, katika hatua ya robo fainali lazima
penati tano tano zipigwe ili kumpata mshindi, ndipo mwamuzi akaamuru penati
hizo zipigwe.
Katika mikwaju hiyo ya penati tano tano, wachezaji
wa Kili Stars Jonas Mkude na Shomari kapombe walishindwa kukwamisha wavuni
penati zao na kuwafanya Wahabeshi hao watinge nusu fainali kwa penati 4-3.
Sasa Ethiopia itavaana na Uganda katika mchezo wa
nusu fainali baada ya Uganda mchana wa leo kuichakaza Malawi mabao 2-0.

0 comments:
Post a Comment