UNAJUA KUWA USHANGILIAJI WA GOLI HUUNGANISHA MATAIFA YOTE DUNIANI?




























KATIKA michezo, mpira unapoingia golini watu wote hushangilia kwa  sauti kubwa, “Goooooooooo!”

Neno hilo limetokana na kifaa kinachowekwa katika pande mbili za uwanja, ambazo ndizo tendo la ufungaji linatendeka.Kifaa hicho kina utofauti wake kulingana na mchezo husika ambapo mchezo wa soka huwa kunakuwa na milingoti mitatu iliyoungana inayosimikwa katika pande mbili za uwanja.

Milingoti ya namna hiyo unaweza pia kuiona kwenye uwanja wa mchezo wa mpira wa mikono, mpira wa magongo nk.Kadhalika katika mchezo wa mpira wa kikapu, kifaa hicho huwa tofauti kidogo ambapo  huwa na muonekano wa duara.

Kifaa hicho pia lazima ukikute katika mchezo wa mpira wa pete ambapo pia huwa na umbo la duara.

ASILI YA NENO ‘GOAL’
Bila kujali kinatumika kwenye mchezo gani, kifaa hiki Waingereza walikipa jina la ‘Goal’ ambalo tafsiri yake ya kawaida ni malengo yanayotimizwa kutokana na juhudi fulani.

Hivyo neno hilo likapelekwa kwenye michezo kwa maana ya kwamba timu inapokuwa uwanjani lazima ifikie malengo kutokana na juhudi inazoonyesha ndani ya uwanja.Hapo ndipo walipotafuta kifaa maalumu na kukipa jina la goal kwa maana kwamba timu lazima ipitishe mpira katika sehemu husika ili kupata suluhu ya juhudi zake.


Vinginevyo timu zote tunazoziona hivi sasa zingekuwa zinapambana tu bila kupata mshindi na mwishowe hata mechi zingekuwa hazina maana yoyote ile.

NENO LIMETOHOLEWA
Mataifa mengi duniani yametohoa neno hili la kiingereza kwenda katika lugha zao ili kupata urahisi wa kulitamka pindi mpira unapoingia langoni.

Lakini licha ya kutohoa na kupata maneno yanayoandikwa kwa lugha tofauti tofauti, matokeo ya mwisho ya utamkaji wake huishia kufanana.

Mataifa yanayozungumza lugha ya kiingereza yakiwemo ya Bara la Afrika, neno ‘goal’hulitamka “Gooooooooo!”. Ndivyo ambavyo pia utasikia nchi kama Hispania, Denmark, Ujerumani pamoja na nchi zingine za Bara la Amerika zikiwa zinatamka hivyo hivyo.

Nchi za Afrika Mashariki ambazo watu wake wanazungumza lugha ya Kiswahili kama Tanzania, nayo imetohoa neno hilo na kuliita ‘goli’.Mashabiki wanaposhangilia kufungwa kwa goli nao hutamka matamshi yanayofanana na mataifa mengine, “Gooooooo!”

Kadhalika nchi kama Kenya na Uganda ambazo baadhi ya watu wake wanazungumza lugha ya Kiswahili, nao linapofungwa goli hushangilia kwa matamshi hayohayo.

GOLAZO
Golazo ni neno ambalo limejizolea umaarufu sana kwa hivi sasa hasa katika nchi za Hispania, Brazil na Colombia.

Kwa mfano goli linapofungwa katika mechi ya mpira wa miguu utasikia mtangazaji akitamka “Gooolaaazoooooooo!”


Neno hilo liliibuka hasa kutoka nchini Hispania likiwa na maana ya goli zuri sana ama goli lililofungwa kwa ustadi mkubwa sana.Kwa mfano mtu anaweza kusema Colombia imemfunga Brazil 2-1 lakini goli la Brazil lilikuwa Golazo.

Lakini neno Golazo mara zote hutamkwa kifupi, yaani “Goooooooooo” badala ya kumalizia ‘Golazooo’.

HELUWA
Neno hili linatumika sana katika nchi za kiarabu hasa baada ya goli kufungwa ambapo watangazaji na mashabiki husikika wakisema “Heluwaaaaaaaaa!”

Heluwa kwa kiarabu ni kitu kizuri sana, hivyo inapotokea goli zuri limefungwa basi hutumia neno hilo.

Licha ya kutumia ‘Heluwa’, kuna wakati wanalazimika kutamka neno “Goooooooooo!”.Mara nyingi haya maneno hutumika kwa pamoja hasa goli linapofungwa katika mchezo wa soka.

Kwa ujumla ushangiliaji wa goli uwanjani huwaunganisha watu pamoja na kuwa kitu kimoja kwa sababu wanatamka kitu kinachofanana.Kwa muda huo hata ubaguzi huwekwa pembeni bila kujali kwamba neno hilo huandikwaje.

Makala haya yameandaliwa na Arone Mpanduka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya mtandao wa Intaneti.
Share on Google Plus

About MPANDUKA BLOG

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment