UMESHAWAHI kumuona mbwa anacheza dansi? Kama
hujawahi kuona ama kusikia basi ukweli ni kwamba mbwa ana uwezo wa kunengua
endapo atafundishwa.
Mchezo huu unafahamika kama Musical canine freestyle
ama freestyle dance ambao umejaa vitu vingi ambavyo mbwa anafundishwa ikiwemo
nidhamu ya mazoezi, mbinu na vionjo vya kunengua.
Katika mchezo huu, mmiliki wa mbwa huwa na uhuru wa
kufundisha mbinu mbalimbali za kucheza muziki.
Mchezo huo umewekwa kwenye mfumo wa mashindano na
umesambaa katika nchi mbalimbali duniani.
HISTORIA
YAKE
Mchezo wa kuwachezesha muziki mbwa ulianza katika
miaka ya 1989 katika nchi ya Canada, Uingereza na Marekani kabla ya baadae
kuenea hadi nchi ya Uholanzi.
Lengo kubwa lilikuwa ni kutengeneza nidhamu kubwa
kwa mbwa wanaowafuga lakini wakaamua kupeleka mbali zaidi na kugeuza kuwa
sehemu ya mashindano.
Chama cha kwanza cha muziki wa mbwa kilikuwa ni cha
kimataifa na kilianzishwa katika nchi za Uingereza, Colombia na Canada mnamo
mwaka 1991.
Baada ya hapo haikuchukua muda sana kwani vyama
vingine vilianzishwa katika nchi za Bara la Amerika.
Kila ukanda ulianza kuendeleza mtindo wake huku
vyama kutoka nchi za Bara la Marekani vikionekana kung’ara zaidi kwa kuongeza
mbinu nyingi zaidi.
Baada ya hapo thamani ya wanyama ikaanza kuonekana
kwa nchi za Ulaya na Marekani ambapo walikuwa wanatumiwa ipasavyo kupitia
mashindano ya ubunifu wa mavazi na hata kucheza muziki.
AINA
ZA DANSI LA MBWA
Zipo aina mbili ambazo mbwa anacheza dansi. Aina ya
kwanza ni ile ambayo mbwa anacheza muziki kwa kutumia visigino vyake na aina ya
pili ni ile ambayo anacheza kwa kutumia mitindo tofauti tofauti.
AINA
YA KWANZA
Katika aina hiyo ya kucheza kwa
kisigino, mbwa lazima awe karibu na mkufunzi wake ili aweze kumpa msaada wa
kushika miguu yake ya mbele na kumfanya acheze kwa kusimama kama binadamu.
Maana yake ni kwamba anaposimama
anakuwa anatumia zaidi visigino vyake.
AINA YA PILI
Katika aina hiyo ambayo hufahamika
kama Musical freestyle, mbwa huwa huru kucheza mwenyewe na kutumia mitindo
mbalimbali na ubunifu wa kila aina.
Hapo mbwa anaweza kutikisa mkia
anavyotaka, kutikisa manyoya yake, kugaa gaa chini na hata kurukaruka.
MASHINDANO
Kwa sasa kuna vyama vingi vya
kimataifa vya mchezo huo vimeanzishwa ambavyo ni pamoja na World Canine
Freestyle Organization, Canine Freestyle Federation na Musical Dog Sport
Association ambacho kipo nchini Marekani.
Kingine
kinaitwa Paws 2 Dance Canine Freestyle Organization cha nchini Canada pamoja na
Pawfect K9 Freestyle Club cha nchini Japan.
Kanuni
na sheria za mashindano hutofautiana kati ya chama na chama na nchi moja na
nyingine.
Hiyo pia inachagizwa na tofauti ya
ubunifu unaotumiwa na kila chama na kila nchi.
Mashindano yanaweza kufanyika kwa kuhusisha mbwa
mmoja ama kundi la mbwa wakiambatana na wakufunzi wao, na kawaida ni kwamba
hata kama kuna mbwa kumi wanashindanishwa, lazima kila mbwa aambatane na
mkufunzi wake.
Pia aina ya mashindano hutegemea na chaguo la muziki
ambao mbwa anacheza kulingana na jinsi walivyopata mafunzo.
Faida kubwa inayopatikana kwa mashindano haya ni
kuingiza kipato kwa nchi husika kwa sababu wapo watu wanaowekeza kwa ajili ya
mashindano hayo.
TOFAUTI
YA MBWA WA ULAYA NA AFRIKA
Katika nchi za Afrika mnyama mbwa bado thamani yake
imekuwa ndogo mno kwa sababu anadharaulika na kuonekana kitu kisicho na maana.
Kinachoonekana ni kwamba Waafrika wengi hawathamini
mbwa ikiwemo kutowapa matunzo stahiki kama vile chakula hasa kwa mfugaji na
badala yake kinachotegemewa zaidi ni huduma ya ulinzi tu.
Kwa bahati nzuri ama mbaya, mchezo wa dansi kwa mbwa
bado haujaingia nchi za Afrika.
Makala haya yameandaliwa na Arone Mpanduka kwa msaada wa mtandao wa Intaneti





0 comments:
Post a Comment