Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeipiga
faini ya sh. 500,000 (laki tano) klabu ya Stand United baada ya timu yake
kupata kadi zaidi ya tano kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Coastal
Union iliyofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Katika mechi hiyo
iliyochezwa Desemba 26, 2015, timu hiyo ilipata kadi saba kinyume na Kanuni ya
42(11) ya Ligi Kuu.
Wachezaji Fred Mbuna wa Majimaji, na Hamad Kibopile
wa Mbeya City watafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) kutokana na kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu wakati wa
mechi kati ya timu zao dhidi ya Azam na Yanga.
Kibopile aliwatolewa waamuzi lugha za kudhalilisha
wakati wa mapumziko kwenye mechi dhidi ya Yanga, huku Mbuna akipiga teke chupa
ya maji, na maji hayo kuwarukia waandishi wa habari wakati wakiripoti mechi
hiyo mjini Songea.
Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano)
kutokana na washabiki wake kumrushia mwamuzi msaidizi namba moja chupa za maji
na makopo ya bia wakipinga kuashiria mshambuliaji wa Simba kuotea dakika ya 57.
Pia walifanya hivyo dakika ya 80 kwenye mechi hiyo dhidi ya Mwadui iliyochezwa
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Timu ya Toto Africans imepewa onyo kwa kuchelewa
uwanjani kwa dakika 23 kwenye mechi yao dhidi ya African Sports iliyofanyika
Desemba 27, 2015 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

0 comments:
Post a Comment