MKUU wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Klabu ya
Simba, Haji Manara amelalamikia tabia ya Mkuu wa Habari wa Yanga Jerry Muro
kuendelea kumpiga vijembe vinavyolenga kumdhalilisha kupitia vyombo vya habari.
Akizungumza hivi karibuni kupitia kituo cha Redio
cha EFM, Manara alikilaumu kituo hicho kwa kumpa muda wa maongezi Jerry ambaye
aliutumia kwa kutoa kauli za kumdhalilisha.
Manara alisema ameumizwa na kitendo cha Jerry
kutamka hewani kwamba amekuwa akiwashwa washwa kwa kufuatilia mambo ya Yanga
ambayo hayamuhusu.
“Anatumia muda mwingi sana kumzungumzia Haji na
maisha yake na cha ajabu mmenisikitisha sana kumruhusu anidhalilishe,
ataniambiaje mimi ninawashwa na nataka kukunwa? Hebu angalieni vitu vingine vya
kurusha hewani.Ni vizuri ndugu yangu akazungumzia zaidi mpira badala ya mtu
binafsi”
“Ninachojaribu kulia na Yanga siku zote si kuisemea
bali ni kuzungumzia uhalisia wa kile kinachoendelea hasa wingi wa mechi zao za
viporo.Duniani kote umeona wapi timu inacheza mechi tatu mfululizo za
viporo?Hiyo ndiyo hoja yangu ya msingi, na siku zote nitabaki kuwa muungwana na
wala sitomjibu,”alisema Manara.
Manara aliyasema hayo ikiwa ni siku moja baada ya
Jerry kutoa kauli hizo hewani huku kisa kikiwa ni uwepo wa mechi nyingi za
viporo za Ligi Kuu kwa Yanga ambayo inashiriki mashindano ya Klabu Bingwa
Afrika.

0 comments:
Post a Comment