Timu ya soka ya Yanga leo(Jumamosi Feb 13) imeanza vizuri kampeni yake
ya mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika baada ya kuinyuka Cercle de Joachim
bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Mauritius.
Bao pekee la ushindi kwa Yanga limefungwa na mshambuliaji
Mzimbabwe, Donald Ngoma.
Ngoma alifunga bao hilo kunako dakika ya 17 akimalizia
krosi maridadi ya beki wa kulia, Juma Abdul Jaffar katika mchezo ambao ulichezeshwa
na marefa wa Madagascar, Hubert Marie Bruno , Ravonirina Harizo na Augustin
Gabriel Herinirina.
Yanga SC ilipata pigo kipindi cha pili, baada ya
mpishi wa bao lake, Juma Abdul Jaffar kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo,
nafasi yake ikichukuliwa na Pato Ngonyani, aliyemalizia vizuri.
Kwa ushindi huo, Yanga SC sasa watakuwa na kazi
nyepesi katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo mjini Dar es Salaam,
wakihitaji hata sare ili kusonga mbele, ambako watakutana na mshindi kati ya
APR ya Rwanda na Mbabane Swallows ya Swaziland.
Baada ya mchezo wa leo, Yanga SC inatarajiwa kupanda
ndege ya ATC waliyokwenda nayo huko, kuelekea kisiwani Pemba kuweka kambi ya
kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu,
Simba SC Jumamosi wiki ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kikosi cha Yanga kiliwakilishwa na kipa Ally Mustafa
'Barthez', Juma Abdul/Pato Ngonyani dk70, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Vincent
Bossou, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Donald Ngoma, Amissi
Tambwe/Paul Nonga dk68 na Deus Kaseke.
0 comments:
Post a Comment