Na Arone Mpanduka
Hatimaye Rais wa klabu ya TP Mazembe ya Congo DR
Moise Katumbi amekubali mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally
Samatta ajiunge na klabu ya Genk ya Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Akizungumza na MPANDUKA BLOG jioni ya leo(Januari
25) baba mzazi wa Mbwana, mzee Ally Samatta amesema kwamba Katumbi ameridhia
Samatta aende klabu anayopenda.
Wiki iliyopita Samatta alisafiri kutoka Tanzania na
kurejea TP Mazembe kwa lengo la kumbembeleza Katumbi abadili msimamo wake wa
kutaka kumpeleka Ufaransa na badala yake akubali dili la Genk ya Ubelgiji.
Kwa kipindi kirefu Katumbi alikuwa anapinga Samatta
kwenda Genk kwa madai kwamba Genk imetaja dau dogo ikilinganishwa na uwezo wa
mchezaji.
“Mwanangu nimemuombea sana kwa Mungu ili mambo yake
yafanikiwe na sasa nafurahi sana kuona sasa bwana mkubwa(Katumbi) amekubali
aende anakotaka,”alisema mzee Ally Samatta.
“Mazungumzo yao yamekamilika leo na kijana wangu
atarejea nchini na kisha atajiandaa na safari ya kwenda Ubelgiji kucheza soka
la kulipwa.Nimefurahi sana”
“Pia niishukuru sana Serikali kwasababu kuna
muwakilishi mmoja wa Serikali alikwenda Congo kumshawishi Katumbi, kitu ambacho
ninafikiri kimeweka uzito wa jambo hili”
MPANDUKA BLOG ilimtafuta Meneja wa Samatta, Jamal
Kisongo kutaka kufahamu kwa undani zaidi juu ya mazungumzo yao jinsi
yalivyokwenda hadi Katumbi akakubali lakini akajibu kwamba suala hilo atatolea
ufafanuzi siku ya Jumatano.
0 comments:
Post a Comment