HIVI karibuni bondia mstaafu Floyd Mayweather
alinunua saa ya mkononi kwa gharama ya dola milioni 1.1 ambayo ni sawa na fedha
za kitanzania zaidi ya bilioni mbili.
Saa hiyo aina ya Hublot inaelezwa kwamba ndiyo ghali
zaidi duniani kwa sasa.
Mayweather alinunua saa hiyo akiwa nchini Dubai
ambako alikwenda kama sehemu ya matembezi yake katika nchi mbalimbali za
kifahari duniani.
Ikumbukwe kuwa Mayweather alipita nchini Uturuki na
pia alikwenda nchini Ufaransa katika matembezi hayo binafsi huku akitumia chopa
yake ya bei ghali.
Saa hiyo ya Hublot ambayo bondia huyo anaimiliki kwa
sasa imetiwa nakshi mbalimbali huku ndani yake kukiwa na kiasi kidogo cha
almasi.
Mayweather ambaye anatoka katika taifa la Marekani
kwa maana kwamba ni raia wa nchi ya Marekani, amenunua saa ambayo thamani yake
inazidi kiwango cha mshahara anacholipwa rais wa Marekani Barack Obama kwa
mwaka.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa mtandao wa Africa Review
uliotolewa mwezi Julai mwaka jana, Obama anapokea mshahara wa kiasi cha dola
400,000 kwa mwaka.
Kwa hesabu za haraka haraka ni kwamba saa ya
Mayweather inaweza kumlipa Obama mshahara wa miaka miwili huku kiasi kingine cha
pesa kikibaki.
Hiyo ni kufuru ya aina yake kwa bondia huyo mstaafu
ambaye amekuwa akitumia pesa kwa fujo bila ya kujali anachokipoteza.
Kwa namna moja ama nyingine pia inaweza kuwa kejeli
kwa Obama ambaye ni Rais wa taifa lake, na si taifa hilo pekee, kwani ni Rais
mwenye nguvu duniani na kufanya watu wamuite mbabe wa dunia.
Kwa nchi zilizoendelea, Obama ndiye anayeongoza kwa
kulipwa kiasi kikubwa cha mshahara akifuatiwa na Stephern Harper wa Canada
anayekunja kiasi cha dola 260, 000 kwa mwaka huku Kansela wa Ujerumani, Angela
Markel akiwa anakunja kiasi cha dola 234,000 kwa mwaka.
Tukirejea kwenye saa ya Mayweather, kama akiamua
kumlipa Harper basi anaweza kumlipa mshahara kwa kipindi cha miaka minne
mfululizo.
Hiyo ni kwa
sababu ukichukua dola milioni 1.1 na kutoa dola 260,000 utagundua kwamba kiasi
kitakachobakia ni kingi mno.
Kwa upande wa Angela Markel, gharama ya saa ya
Mayweather inaweza kumlipa mshahara kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo,
tena bila wasiwasi wowote.
Mbali na hilo Mayweather kwa kutumia gharama ya saa
yake anaweza kuwalipa mshahara wa mwaka mmoja vigogo hao watatu kwa mara moja.
Hiyo ni kwa sababu ukijumlisha mshahara wa Obama,
Harper na Markel unapata jumla ya dola 894,000 ambazo si jambo gumu kuwalipa
wote watatu.
KUFURU
ZINGINE ZA MAYWEATHER
Mwezi Januari mwaka huu Mayweather alipiga picha
akiwa mbele ya ndege yake binafsi na
magari manane ya thamani kubwa anayoyamiliki.
Mayweather, anayetajwa kumiliki utajiri wenye
thamani ya pauni milioni 66.1, imeelezwa kuwa thamani ya magari yote manane anayoyamiliki
ni pauni milioni tano.
Mali zote hizo aliamua kuzipiga picha na kusambaza
kwenye mitandao ya kijamii.
Pia aliwahi kutumia pauni 17,000 (zaidi ya milioni
40 za kitanzania) kwa ajili ya vifaa vya kukinga kinywa (gum shield) katika
pambano lake dhidi ya Manny Pacquiao lililofanyika kwenye ukumbi wa Las Vegas,
Marekani Mei 2 mwaka huu.
Aliamua kutumia gharama kubwa kutengeneza vifaa
hivyo kwa kutumia dhahabu, vumbi la almasi na vipande vya fedha halisi, vyote
vikichanganywa katika plastiki na kuandikwa jina lake.
Bondia huyo alisema amelazimika kutengeneza vifaa
hivyo vya kifahari kwa madai kwamba vitalinda meno yake na kumsaidia kupumua
vizuri wakati wa pambano.
mpanduka@yahoo.com
0786 160643
0 comments:
Post a Comment