FRED MOSHA KUZIKWA JUMATATU DAR



Na Arone Mpanduka

Mwili wa mwanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini TASWA, Fred Mosha unatarajiwa kuzikwa Jumatatu ya Februari 22 mwaka huu kwenye makaburi ya Kinondoni jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu, maziko yatafanyika saa 10 jioni.

Msiba upo nyumbani kwake Mbagala Saku kwa Mkongo jijini Dar es salaam.
Fred Mosha ambaye ni mmoja wa waasisi wa vipindi vya michezo vya Redio Tumaini amefariki kwenye hospitali ya Muhimbili alfajiri ya leo baada ya kuugua saratani ya shingo kwa muda mfupi.

Hadi umauti unamkuta Fred alikuwa ni Mkuu wa Kitengo cha habari cha Tumaini Media, yaani Redio na TV Tumaini.

Marehemu Fred Mosha atakumbukwa kwa mengi ikiwemo uchambuzi wa nyimbo za zamani kutoka Redio Tumaini, kipindi ambacho kilikuwa kinaruka kila siku za Jumamosi kuanzia saa tano asubuhi hadi saa saba mchana.

Ni miongoni mwa waasisi wa vipindi vya michezo mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Alikuwa ni mjuzi wa mambo mengi kwani alikuwa na uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu na kuchambua siasa, muziki na michezo na kupelekea watu kumpa jina la utani la google.

Fred Mosha alikuwa ni mmoja kati ya watangazaji waliobuni na kushiriki staili ya kutangaza soka la Ulaya kwa njia ya TV.

Hiyo ilifanywa kwa mara ya kwanza na Redio Tumaini kwenye fainali za kombe la dunia la mwaka 1998.

Watangazaji wa fainali hizo wakati huo walikuwa ni Fred mwenyewe, Tom Chilala na Victor Robert Wille.

Mchambuzi alikuwa ni kocha Joseph Kanakamfumo.

Baada ya hapo media zingine zikafuata staili hiyo.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina!
Share on Google Plus

About MPANDUKA BLOG

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Post a Comment