Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa, Sepp
Blatter amelazwa hospitalini kutokana na kupatwa mshituko wa neva.
Blatter (79) aliyesimamishwa kwa siku 90
kujishughulisha na masuala ya soka wakati akichunguzwa kwa kashfa ya kutoa
mlungula, alilazwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa afya lakini sasa
imeelezwa atakaa zaidi humo.
Mwanamichezo huyo aliyeongoza ulimwengu wa soka kwa
miaka 18 sasa, awali ilidaiwa alikuwa na matatizo ya msongo wa mawazo hivyo
ikabidi apate huduma ya matabibu, sasa imebainika ana tatizo la mshituko wa
neva.
Awali, mwanasheria wake, Richard Cullen alieleza juu
ya uangalizi huo wa madaktari kutarajiwa, lakini akawa amesema alitarajia
arejee nyumbani mapema kabla hali kubadilika na kutolewa maelezo tofauti.
Hata hivyo, maswahiba wake wameeleza kwamba hali
yake si mbaya na anatarajiwa kurejea katika hali ya kawaida japokuwa atabaki
hospitalini hadi mapema wiki ijayo. Blatter amesimamishwa kazi hizo sambamba na
Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini kwa tuhuma za makosa
yanayohusiana.
Imeelezwa kwamba Blatter amekuwa katika kupambana
dhidi ya uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Fifa kumsimamisha kazi na alinukuliwa
akiwaambia rafiki zake kwamba hakuna kamati yoyote ile inayoweza kumweka nje ya
utawala wa Fifa.
Msaidizi wake, Walter Gagg, amesema kwamba bosi huyo
anatarajiwa kuwa mwenyeji wa hafla ya kukabidhi tuzo ya Mwanasoka Bora – Ballon
d’Or jijini Zurich, Januari 11 akimaanisha kwamba atakuwa timamu lakini pia
hana doa kuhusu tuhuma anazohusishwa nazo.
Katikati ya sakata hilo ni shauri la jinai linalomlenga
Blatter na Platini, kwamba Blatter alitumia vibaya pauni milioni 1.35 kumpa
Platini kama hongo mwaka 2011 ili ajitoe kwenye kugombea urais wa Fifa wakati
huo.
Wawili hao wanakana, wakidai hayo yalikuwa malipo
halali kwa Platini, kutokana na kazi ya ushauri wa ufundi kwa rais huto wa Fifa
aliyokuwa ameifanya.
Inashangaza kuona kwamba malipo yalifanyika karibu mwaka
mzima baada ya kazi kumalizika, na muda mfupi tu kabla ya uchaguzi wenyewe
ambao Platini alijiondoa mara na Blatter akashinda.
Uchaguzi wa rais unafanyika Februari mwakani, baada
ya Blatter aliyechaguliwa tena Mei mwaka huu kuamua kuachia ngazi wakati huo
ukifika, kwa maelezo kwamba si ulimwengu wote wa soka unaomuunga mkono.
0 comments:
Post a Comment