Hali imeendelea kuwa mbaya kwa timu ya soka ya Yanga
baada ya hii leo(Julai 16) kuambulia sare katika mchezo wake wa tatu wa hatua ya makundi
ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Medeama ya nchini Ghana.
Mchezo huo ambao umepigwa kwenye dimba la Taifa jijini
Dar es salaam jioni ya leo, Yanga imeambulia sare ya bao 1-1 na kuifanya iwe na
wakati mgumu katika kundi lake la A hasa ikizingatiwa kwamba tayari ilipoteza
mechi mbili za mwanzo.
Donald Ngoma alianza kuifungia Yanga bao la kuongoza
dakika ya kwanza ya mchezo huo akitumia vema makosa ya safu ya ulinzi ya
Medeama na kuiweka timu yake mbele ya Medeama kwa bao 1-0.
Medeama walisawazisha bao hilo dakika ya 17 baada ya
Bernard Danso kuunganisha mpira wa kona na kufanya matokeo kuwa 1-1 ambayo
yalidumu hadi dakika 90 zinamalizika.
Yanga inaendelea kusalia katika nafasi ya mwisho
kwenye kundi lake ikiwa na pointi moja baada ya kucheza mechi tatu bila ushindi
huku ikiwa imepoteza mechi mbili.
Yanga ilifungwa goli 1-0 ugenini na MO Bejaiya ya
Algeria kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi A kabla ya kukubali kichapo kingine
kwenye uwanja wake wa nyumbani dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
0 comments:
Post a Comment